Mzee Tshisekedi, kinara wa upinzani Kongo DR aaga dunia

Kiongozi mkongwe wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mzee Etienne Tshisekedi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84 usiku wa kuamkia leo nchini Ubelgiji.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, Tshisekedi alielekea mjini Brussels nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu ya kiafya mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari.

Hadi tunaenda mitamboni, familia na watu wa karibu na mwanasiasa huyo mkongwe wa DRC walikuwa hawajatoa taarifa yoyote kuhusu ugonjwa wala kifo cha Tshisekedi.

Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka jana 2016, Tshisekedi alirejea Kinshasa kutoka Ubelgiji alikokwenda kwa ajili ya matibabu miaka miwili iliyopita. Maelfu ya wafuasi wake walifurika katika uwanja wa ndege na vilevile kujipanga katika barabara ya kuelekea kwao Limete kumlaki kiongozi huyo mkongwe wa upinzani ambaye kurejea kwake nchini kulitazamiwa kupiga jeki harakati za wapinzani.

AFP imeripoti kuwa, Mzee Tshisekedi ameaga dunia katika hali ambayo, chama chake kinaendelea na mazungumzo ya kugawana mamlaka kufuatia hatua ya Rais Joseph Kabila kukataa kujiuzulu baada ya muda wake wa uongozi kumalizika mwezi uliopita.

Wadadisi wa mambo wanasema Tshisekedi alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe na shupavu na ambao walikuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia katika nchi hiyo ya Kiafrika, na kufa kwake kumeacha pengo kubwa katika medani ya kisiasa sio tu katika nchi hiyo, bali pia kieneo.